Menu

Hosea 14

ONMM

1 Rudi, ee Israeli, kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako. Dhambi zako zimekuwa anguko lako! 2 Chukueni maneno pamoja nanyi, mkamrudie Mwenyezi Mungu. Mwambieni: “Samehe dhambi zetu zote na utupokee kwa neema, ili tuweze kutoa matunda yetu kama sadaka za mafahali. 3 Ashuru hawezi kutuokoa, hatutapanda farasi wa vita. Kamwe hatutasema tena ‘miungu yetu’ kwa kile ambacho mikono yetu wenyewe imetengeneza, kwa kuwa kwako wewe yatima hupata huruma." 4 “Nitaponya ukaidi wao na kuwapenda kwa hiari yangu, kwa kuwa hasira yangu imeondoka kwao. 5 Nitakuwa kama umande kwa Israeli; atachanua kama yungiyungi. Kama mwerezi wa Lebanoni atashusha mizizi yake chini; 6 matawi yake yatatanda. Fahari yake itakuwa kama mti wa mzeituni, harufu yake nzuri kama mwerezi wa Lebanoni. 7 Watu wataishi tena kwenye kivuli chake. Atastawi kama nafaka. Atachanua kama mzabibu, nao umaarufu wake utakuwa kama divai inayotoka Lebanoni. 8 Ee Efraimu, nina shughuli gani tena na sanamu? Nitamjibu na kumtunza. Mimi ni kama msunobari wenye majani mabichi; kuzaa kwako matunda kunatoka kwangu." 9 Ni nani mwenye hekima? Atayatambua mambo haya. Ni nani mwenye ufahamu? Huyu atayaelewa. Njia za Mwenyezi Mungu ni adili; wenye haki huenda katika njia hizo, lakini waasi watajikwaa ndani yake.

Everything we make is available for free because of a generous community of supporters.

Donate