Yeremia 47
ONMM1 Hili ndilo neno la Mwenyezi Mungu lililomjia nabii Yeremia kuhusu Wafilisti, kabla Farao hajaishambulia Gaza: 2 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Tazama jinsi maji yanavyoinuka huko kaskazini, yatakuwa mafuriko yenye nguvu sana. Yataifurikia nchi na vitu vyote vilivyo ndani yake, miji na wanaoishi ndani yake. Watu watapiga kelele; wote wanaoishi katika nchi wataomboleza 3 kwa sauti ya kwato za farasi wanaoenda mbio, kwa sauti ya magari ya vita ya adui, na mngurumo wa magurudumu yake. Baba hawatageuka kuwasaidia watoto wao, mikono yao italegea. 4 Kwa maana siku imewadia kuwaangamiza Wafilisti wote na kuwakatilia mbali walionusurika wote ambao wangeweza kusaidia Tiro na Sidoni. Mwenyezi Mungu anakaribia kuwaangamiza Wafilisti, mabaki toka pwani za Kaftori . 5 Gaza atanyoa kichwa chake katika kuomboleza, Ashkeloni atanyamazishwa. Enyi mabaki kwenye tambarare, mtajikatakata wenyewe hadi lini? 6 “Mnalia, ‘Aa, upanga wa Mwenyezi Mungu, utaendelea hadi lini ndipo upumzike? Rudi ndani ya ala yako; acha na utulie.’ 7 Lakini upanga utatuliaje wakati Mwenyezi Mungu ameuamuru, wakati ameuagiza kuishambulia Ashkeloni pamoja na pwani yake?"
