Zaburi 4
ONMM1 Nijibu nikuitapo, Ee Mungu wangu mwenye haki! Nipumzishe katika shida zangu; nirehemu, usikie ombi langu. 2 Enyi watu, mtabadilisha utukufu wangu kuwa aibu hadi lini? Mtapenda udanganyifu na kufuata miungu ya uongo hadi lini? 3 Fahamuni hakika kwamba Mwenyezi Mungu amewatenga wale wamchao kwa ajili yake; Mwenyezi Mungu atanisikia nimwitapo. 4 Katika hasira yako, usitende dhambi. Tulieni kimya mkiwa vitandani mwenu, mkiichunguza mioyo yenu. 5 Toeni dhabihu zilizo haki; mtegemeeni Mwenyezi Mungu. 6 Wengi wanauliza, “Ni nani awezaye kutuonesha jema lolote?” Ee Mwenyezi Mungu, tuangazie nuru ya uso wako. 7 Wewe umejaza moyo wangu kwa furaha kubwa kuliko watu waliopata nafaka na divai kwa wingi. 8 Nitajilaza chini na kulala kwa amani, kwa kuwa wewe peke yako, Ee Mwenyezi Mungu, waniwezesha kukaa kwa salama.
