Zaburi 8
ONMM1 Ee Mwenyezi Mungu, Bwana wetu, tazama jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani kote! Umeuweka utukufu wako juu ya mbingu. 2 Midomoni mwa watoto wachanga na wanaonyonya umeamuru sifa, kwa sababu ya watesi wako, kumnyamazisha adui na mlipiza kisasi. 3 Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako, mwezi na nyota, ulizoziratibisha, 4 mwanadamu ni kitu gani hata unamfikiria, binadamu ni nani hata unamjali? 5 Umemfanya chini kidogo kuliko viumbe wa mbinguni, ukamvika taji la utukufu na heshima. 6 Umemfanya mtawala juu ya kazi za mikono yako; umeweka vitu vyote chini ya miguu yake. 7 Mifugo na makundi yote pia, naam, na wanyama wa kondeni, 8 ndege wa angani na samaki wa baharini, naam, kila kinachoogelea katika njia za bahari. 9 Ee Mwenyezi Mungu, Bwana wetu, tazama jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani kote!
