Zaburi 16
ONMM1 Ee Mungu, uniweke salama, kwa maana kwako nimekimbilia. 2 Nilimwambia Mwenyezi Mungu, “Wewe ndiwe Bwana wangu; pasipo wewe sina jambo jema." 3 Kuhusu watakatifu walio duniani, hao ndio wenye fahari, na ninapendezwa nao. 4 Huzuni itaongezeka kwa wale wanaokimbilia miungu mingine. Sitazimimina sadaka za damu kwa miungu kama hiyo, au kutaja majina yao mdomoni mwangu. 5 Mwenyezi Mungu umeniwekea fungu langu na kikombe changu; umeyafanya mambo yangu yote yawe salama. 6 Alama za mipaka zimeniangukia mahali pazuri, hakika nimepata urithi mzuri. 7 Nitamsifu Mwenyezi Mungu ambaye hunishauri, hata wakati wa usiku moyo wangu hunifundisha. 8 Nimemweka Mwenyezi Mungu mbele yangu daima. Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume, sitatikisika. 9 Kwa hiyo moyo wangu unafurahia, na ulimi wangu unashangilia; mwili wangu nao utapumzika salama, 10 kwa maana hutaniacha Kuzimu , wala hutamwacha Mtakatifu Wako kuona uharibifu. 11 Umenijulisha njia ya uzima; utanijaza na furaha mbele zako, pamoja na furaha ya milele katika mkono wako wa kuume.
