Zaburi 28
ONMM1 Ninakuita wewe, Ee Mwenyezi Mungu, Mwamba wangu; usikatae kunisikiliza. Kwa sababu ukinyamaza nitafanana na walioshuka shimoni. 2 Sikia kilio changu nikikuomba unihurumie, ninapokuita ili unisaidie, ninapoinua mikono yangu kuelekea Patakatifu pa Patakatifu pako. 3 Usiniburute pamoja na waovu, pamoja na hao watendao mabaya, ambao huzungumza na majirani zao maneno mazuri, lakini mioyoni mwao wameficha chuki. 4 Walipe sawasawa na matendo yao, sawasawa na matendo yao maovu; walipe sawasawa na kazi za mikono yao, uwalipe wanavyostahili. 5 Kwa kuwa hawaheshimu kazi za Mwenyezi Mungu, na yale ambayo mikono yake imetenda, atawabomoa na kamwe hatawajenga tena. 6 Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, kwa maana amesikia kilio changu nikimwomba anihurumie. 7 Mwenyezi Mungu ni nguvu zangu na ngao yangu, moyo wangu umemtumaini yeye, nami nimesaidiwa. Moyo wangu unarukaruka kwa furaha nami nitamshukuru kwa wimbo. 8 Mwenyezi Mungu ni nguvu ya watu wake, ngome ya wokovu kwa mpakwa mafuta wake. 9 Waokoe watu wako na uubariki urithi wako; uwe mchungaji wao na uwabebe milele.
