Zaburi 29
ONMM1 Mpeni Mwenyezi Mungu, enyi mashujaa, mpeni Mwenyezi Mungu utukufu na nguvu. 2 Mpeni Mwenyezi Mungu utukufu unaostahili jina lake; mwabuduni Mwenyezi Mungu katika uzuri wa utakatifu wake. 3 Sauti ya Mwenyezi Mungu iko juu ya maji; Mungu wa utukufu hupiga radi, Mwenyezi Mungu hupiga radi juu ya maji makuu. 4 Sauti ya Mwenyezi Mungu ina nguvu; sauti ya Mwenyezi Mungu ni tukufu. 5 Sauti ya Mwenyezi Mungu huvunja mierezi; Mwenyezi Mungu huvunja vipande vipande mierezi ya Lebanoni. 6 Hufanya Lebanoni irukaruke kama ndama, Sirioni urukaruke kama mwana nyati. 7 Sauti ya Mwenyezi Mungu hupiga kwa miali ya radi. 8 Sauti ya Mwenyezi Mungu hutikisa jangwa; Mwenyezi Mungu hutikisa Jangwa la Kadeshi. 9 Sauti ya Mwenyezi Mungu huzalisha ayala, na huuacha msitu wazi. Hekaluni mwake wote wasema, “Utukufu!" 10 Mwenyezi Mungu huketi akiwa ametawazwa juu ya gharika; Mwenyezi Mungu ametawazwa kuwa Mfalme milele. 11 Mwenyezi Mungu huwapa watu wake nguvu; Mwenyezi Mungu huwabariki watu wake kwa kuwapa amani.
